JINSI YA KUISHI NA MWANAUME ASIYEKUWA NA PESA! - Bongo Loves

JINSI YA KUISHI NA MWANAUME ASIYEKUWA NA PESA!



MUNGU ni mwema! Ni Jumatatu nyingine tunakutana kwenye ulimwengu wetu wa mahaba. Uwanja wetu maridhawa wa kupeana darasa kuhusu maisha na uhusiano. Kama mada inavyojieleza hapo juu, ulimwengu wa sasa wanawake wengi wanaamini katika kuishi na wanaume wenye pesa.
Mwanaume ambaye atakuwa na ukwasi wa kutosha huyo ndiye anayefaa kuwa naye kwenye uhusiano au hata ndoa. Anaamini kwamba pesa ndiyo kila kitu. Pesa ndiyo itakayompa mahitaji yake ya kupendeza na kila kitu. Mwanaume bila pesa kwake ni sawa na debe tupu. Upepo wa imani hiyo upo sana mjini.
Kule vijijini jambo hilo lipo, lakini si kwa kiasi kikubwa. Wanawake wa mjini huwaambii kitu kuhusu suala la kupendeza. Gharama za kupendeza ni kubwa. Mtu hata kama hana kazi atalazimika tu kufanya lolote lile ili tu aendane na wanawake wengine wa mjini, asionekane mshamba. Ndugu zangu wanawake, maisha ya sasa yamebadilika hivyo ni vyema na ninyi mkaanza kuendana na wakati. Kubadilisha mawazo na kuamini kwamba, pesa siyo kila kitu. Pesa ni kwa ajili ya mahitaji, lakini kuna suala la msingi sana unalopaswa kulizingatia. Unapoingia kwenye uhusiano na mtu, angalia sana ubinadamu.
Angalia upendo wa dhati, angalia hofu ya Mungu, angalia sana uvumilivu, angalia moyo wa mtu ukoje. Si kila mwenye pesa basi ana hivyo vitu nilivyovianisha. Unaweza kuingia kwenye uhusiano na mtu mwenye pesa, lakini mwisho wa siku ukaenda kuvikosa hivyo vitu na ukaishia kuteseka. Ukaishia kunyanyaswa au kuonewa na huyo mtu. Maisha yako yote yanaweza kuwa machungu kwa sababu tu ya tamaa ya pesa. Mimi na wewe leo hii ni mashahidi wa jambo hili kwani tunayashuhudia mitaani.
Baadhi ya wanawake wanaolewa na watu wenye pesa, lakini matokeo yake wanageuka kuwa watumishi wa nyumbani wa hao wanaume wao. Wanageuka kuwa wafanyakazi wa ndani na si wake tena. Wanakosa sauti ya kusema, lakini mioyoni wanabeba mambo mazito yanayofukuta kama moto. Hawazifurahii ndoa zao, wanaambulia masimango, manyanyaso ya kila aina maishani mwao. Hii ni hatari sana! Unaweza kuishi na mwanaume asiyekuwa na pesa, lakini
kipaumbele kikubwa kiwe ni mambo niliyoyataja hapo juu. Ishi na mtu ambaye hata kama hana pesa, lakini ana utu, ana ubinadamu na hofu ya Mungu. Kikubwa zaidi angalia mwanaume ambaye anajielewa. Anayejitambua, anayeamini katika kutafuta maisha. Kwamba hata kama hana pesa, lakini akili yake iamini katika kutafuta. Kama hiyo akili, mwanamke ni jukumu
lako kumkumbusha. Mweleze mwanaume wako juu ya umuhimu wa kutafuta. Wekeni mipango ya pamoja, mnapowaza pamoja juu ya changamoto zenu hakuna kitakachowashinda. Baadhi ya wanaume huwa ni wazito
kuwashirikisha wanawake wao mambo ya kimaendeleo. Mshtue mwanaume wako kuhusu masuala ya kimaendeleo. Mjengee utaratibu wa kuzungumza kuhusu fursa mbalimbali zenye mtaji mdogo na hata mkubwa. Zile zenye mitaji mikubwa mnaweza kuzifikia pale mtakapofanikisha zile za mitaji midogo. Mnachotakiwa ni kufurahia maisha yenu. Kuyakubali na kupanga mikakati ya pamoja ya kuelekea kwenye maisha mnayoyatamani.
Msiyumbishwe na pesa, mtakapozipata pia zisiwazuzue kwani upendo wenu, utu wenu ulikuwa na maana kubwa kabla hata hamjaziapata pesa. Mikiishi hivyo na mkamtanguliza Mungu katika safari yenu, hakuna gumu litakalowashinda. Zaidi mtadumisha upendo wenu, kila kitu kitaenda vizuri! Instagram na Facebook: Erick Evarist, Twitter: ENangale.
USISAHAU KUSHARE NA KUCOMMENT APPLICATION YETU YA KONA YA MAHABA❤️😘😍 https://play.google.com/store/apps/details?id=tz.konayamahaba.app&hl=en

0 Response to "JINSI YA KUISHI NA MWANAUME ASIYEKUWA NA PESA!"

Post a Comment