HAKUNA kitu kinauma kama kuachwa. Anayeachwa huwa anakuwa hayupo tayari kukubali matokeo. Aliyemuacha mwenzake anakuwa amejiandaa wakati mwenzake hajajiandaa. Ni rahisi sana kwa aliyeachwa kutengeneza chuki kwa aliyemuacha. 

Ndiyo maana wengi sana wanapoachana huwa wanageuka maadui. Mtu hataki kabisa kushirikiana na mwenzake kwa chochote. Hata kama suala wanalo-zungumza ni la kawaida, yuko radhi atafute mtu mwingine azungumze naye na si aliyekuwa mpenzi wake.

SIKILIZA KISA HIKI:
John na Maria walikuwa wapenzi kwa muda mrefu. Penzi lao liliota mizizi kwa maana ya kuwagusa marafiki zao wa karibu. Lilienda mbele pia kwa kuhusisha baadhi ya ndugu wakiwemo madada na kaka wa pande zote mbili.

Kama hiyo haitoshi, penzi hilo pia liliwagusa mama wa pande zote mbili ambao waliujua uhusiano wao. Walitamani kuwaona wakiwa kama mke na mume lakini wawili hao ndoto zao ziliishia njiani. Kila mmoja akachukua hamsini zake.
Matokeo yake, John na Maria wakawa maadui. Maria ambaye hakujiandaa kuachwa, hakutaka hata kuwasalimia marafiki wa John. Hakutaka hata kuwasogelea maana aliamini wangemuongezea machungu. Aliwaona nao kama maadui zake. Aliwachukia kwelikweli.

Baadaye hata mama, kaka na dada wa John aliwaona kama kituo cha polisi. Akafuta namba ya simu ya John, hakutamani kumuona mahali popote, kifupi hakutaka kuona hata mafanikio yake. Alimuombea mabaya.

TUNAJIFUNZA NINI HAPO?
Kweli hakuna anayefurahia kuachwa. Mapenzi yanauma, wakati mwingine hasira zinaweza kutuongoza katika kufanya maamuzi lakini suala la msingi linalopaswa kuzingatia ni kujidhibiti. Lazima tujifunze kudhibiti hasira zetu.

Kuachwa au kuachana siyo mwisho wa maisha. Kweli mnaweza kuwa mmewekeza nguvu, ndugu na hata marafiki katika uhusiano wenu lakini endapo imetokea mmeshindwa kuendelea na safari kwa namna moja au nyingine basi hakuna budi kushukuru na kuliacha lipite.

Usimuone mwenzako kama adui bali chukulia kama changamoto katika maisha yako kwani hujui pengine ni nini kingetokea kama ungeendelea na safari hiyo. Yawezekana Mungu amekuepusha na jambo lingine zito huko mbeleni.

Mshukuru yeye, usiwachukie marafiki, usiwakasirikie ndugu zake wala yeye mwenyewe. Mchukulie kama tu alikuwa mpenzi wako. Mheshimu maana pia anazo siri zako nyingi. Anakujua vizuri hivyo kama itakupendeza pia muombee mafanikio.

Muombe naye akuombee pia wewe katika safari yako. Kama una shida ambayo unaona yeye anaweza kuwa msaada kwako, mueleze. Kama atakuwa ni muungwana anaweza kukusaidia. Zungumza na marafiki na ndugu zake kama vile hakuna kitu chochote kilichotokea.
Yawezekana hili likakushinda katika kipindi cha awali lakini jipe moyo. Baadaye utaweza. Msalimie ukimuona barabarani. Hii inakufanya uonekane mstaarabu hata kwa ndugu zake hivyo itakuwa jambo jema pia kwao hata kuweza pia kufufua upya penzi lenu.

Kuna fursa ambazo anaweza kukupa au wewe ukampa hata kama mmetengana. Weka uhusiano pembeni, ruhusu moyo wako uwe katika hali ya urafiki. Urafiki utakupa fursa nyingi na endapo yeye au wewe utampata mwenza basi mtaambizana.

Kila mmoja atakuwa huru na hapo kidogo mawasiliano yanaweza kupungua ili kuepuka migogoro na wenza wenu wapya lakini inapowezekana mnaweza kusalimiana. Hayo ndiyo maisha na hakuna sababu ya kuwekeana chuki katika dunia hii iliyojaa nafasi nyingi maishani.