Unaweza Kumruhusu Mtoto Afuate Dini Apendayo?
Ipo nafasi muhimu ya
imani/dini katika malezi ya watoto. Imani si tu inamsaidia mtoto kujitambua,
lakini pia ina nafasi ya kumtengenezea mtoto sauti kutoka ndani yake inayomsaidia
kupambanua lililo jema na baya. Sauti hii inaitwa dhamira.
Utakuwa shahidi kuwa kuna
mambo wakati mwingine unatamani kuyafanya lakini unajisikia hatia kuyafanya.
Unaweza, kwa mfano, kuwa na uhuru wa kutaka kufanya chochote, lakini kuna sauti
ndani yako ikakunyima ujasiri wa kukifanya. Hakuna anayekuona, hakuna
anayekuhukumu, lakini kuna kengele ndani yako inakwambia kuwa unachotaka
kukifanya sio sahihi.
Mwanasaikolojia wa kale
anayeitwa Sigmund Freud aliita kengele hiyo ‘Superego’ kumaanisha mkusanyiko wa
maelekezo tunayoyapata kwa watu wanaotuzunguka. Kwa kawaida, sauti na maelekezo
hayo inayoumbika ndani yetu ndiyo inayoamua namna gani tunadhibiti matamanio
yetu ya asili kama hasira na tamaa za mwili.
Imani, tafiti zinasema, ina
kazi kubwa ya kujenga dhamira. Mtu mwenye dhamira iliyojengwa sawa sawa anakuwa
na uwezo mzuri wa kupambanua lililo jema na baya. Kwa mfano, watoto waliolelewa
kwenye misingi imara ya kiimani/kidini, wana uwezekano mkubwa zaidi wa kuwa na
nidhamu, kufikiria mahitaji ya wengine, na hata kuchelewa kuanza kushiriki
mapenzi ukilinganisha na watoto wasio na mizizi yoyote ya kiimani/kidini.
Nakumbuka nikiwa na umri
wa miaka kama mitano na kuendelea baba yangu alikuwa na utaratibu
tuliouchukulia kama desturi ya nyumbani. Kila jioni ilikuwa ni sharti mimi na
wadogo zangu wawili tukutane nae sebuleni kufanya ibada ya pamoja. Katika ibada
hizo, tuliimba, tulisali, na kusikiliza hadithi zilizotokana na mafundisho ya
biblia.
Mzee alitumia hadithi
kutufundisha mambo mengi yanayohusu imani na maadili. Kipindi hicho, miaka ya
80 hapakuwa na televisheni nyumbani isipokuwa radio. Hadithi hizo zilikuwa
mithili ya tamthlia za leo zilizoanza tangu nyakati za uumbaji, Adamu na Hawa
katika bustani ya Eden, historia ya Uyahudi ya kale mpaka maisha ya Bwana Yesu
Kristo. Kila baada ya masimulizi hayo yaliyonukuu vifungu vya biblia,
tulijifunza namna gani mambo hayo yalihusianishwa na maisha yetu kama watoto.
Tulisisimuka kweli kweli kama watoto.
Sauti ya mzee haikuondoka
kwenye ufahamu wangu. Kila mara katika utoto na ujana wangu ningeweza kumsikia
akizungumza na mimi. Hata hivi leo, kuna nyakati ninapofanya maamuzi ya
kimaisha, nakumbuka sauti niliyozoea kuisikia zaidi ya miaka 30 iliyopita. Hiki
ndicho ambacho Sigmund Freud alikiita ‘superego.’
Hata hivyo, kuna
changamoto ya kutofautisha dini na imani. Wakati imani ni maisha ya kiroho
aliyonayo mtu, dini ni suala la kitaasisi zaidi. Ndio kusema unaweza kuwa na
dini lakini ndani yako pasiwe na sauti dhahiri inayoongoza uhusiano wako na
Mungu.
Wengi wetu tulilelewa
kidini lakini si kiimani. Tulifundishwa kutii taratibu zinazoongoza dini zetu
lakini hatukujua kwa hakika kile tunachokiamini. Sasa tumekuwa wazazi, nasi tunafanya yale
yale. Tunawarithisha watoto dini zetu na kusahau maisha yao ya kiroho. Matokeo
yake, tunashuhudia watoto wengi wakifanya mambo yasiyo ya adili na tunashangaa
imekuwaje.
Je, tunaweza kuwafundisha
watoto wetu imani kwa maana ya kuwakuza kiroho badala ya kushika dini? Je,
unaweza kumruhusu mwanao kutafuta imani nje ya dini yako?
0 Response to " Unaweza Kumruhusu Mtoto Afuate Dini Apendayo?"
Post a Comment