Mazingira Yanayoweza Kuanzisha Mapenzi Yasiyotarajiwa Kazini
Dorcas, msichana wa miaka 30 anayefanya kazi kama Afisa Mikopo
kwenye benki moja mjini, hakuwahi kufikiri ingetokea siku moja ‘achepuke’
kimapenzi na Johnson ambaye ni mfanyakazi mwenzake. Miaka mitatu iliyopita
wakati anaanza kazi kwenye benki hiyo, Dorcas alikuwa na msimamo thabiti na
aliheshimu ndoa yake.
Ingawa alifanya kazi kwa karibu na Johnson, Dorcas hakumchukulia
kama mtu mwenye sifa stahiki za kumvutia kimapenzi. Kilichotokea mwaka mmoja
baadae, kwa mujibu wa Dorcas, hakieleweki. Dorcas si tu amejikuta kwenye penzi
zito na Johnson, lakini amejikuta akichafua sifa yake na kuhatarisha kazi yake.
Ingawa mapenzi ofisini huwaathiri wahusika wote wawili, mara
nyingi mwathirika mkubwa huwa ni mwanamke. Kisaikolojia, mwanamke huchukulia
mapenzi kwa hisia na uzito zaidi kuliko mwanaume. Pia inapotokea wawili hao wamebainika,
jamii yetu humwadhibu mwanamke kwa maneno na hisia kuliko mwanaume.
Sote tunafahamu hatari ya mapenzi kazini. Mbali na kupoteza kazi
ukiingia pasipoingilika, unaweza kuharibu sifa yako, ukapoteza furaha ya kazi
na hata kuvuruga ndoa/mahusiano uliyonayo. Jambo la kujiuliza, hata hivyo, ni
kwa nini watu ambao awali wasingedhani wangejikuta kwenye lindi la mapenzi na
wasiyemtarajia, hujikuta katika mazingira ambayo hawawezi tena kujizuia?
Mazoea ya kikazi
Wafanyakazi wengi hujikuta wakijiwa na hisia za kimapenzi na
wafanyakazi wenzao kwa sababu ya kutumia muda mwingi pamoja. Dorcas anaeleza
jambo hili vizuri. ‘Hata sijui ilikuwaje. Sikujua kinachoendelea hata. Tulikuwa
tunafanya kazi pamoja kwa muda mrefu. Nikaanza kupenda kazi yake. Nikaanza
kuvutiwa na bidii yake kazini. Basi nikajikuta nampenda.’
Ofisi inaweza kuwa bustani ya mapenzi. Kufanya kazi kwa karibu na
kwa muda mrefu pamoja kunaweza kuzalisha hisia zisizotarajiwa kama ilivyotokea
kwa Dorcas.
‘Tulifanya kazi kwa karibu sana,’ anasimulia. ‘Unajua kipindi
hicho sikuwa nafahamu vizuri kazi. Johnson ndio akawa msaada wangu pale
ofisini. Wakati mwingine tulikaa mpaka usiku tukikimbizana na deadline (saa ya
kukabidhi kazi)…kidogo kidogo nikaanza kumpenda.’
Pamoja na umuhimu wa kufanya kazi kwa ukaribu na wenzako, ni
muhimu kujiwekea misimamo itakayokulinda. Epuka kuweka mazingira ya urafiki wa
karibu na wafanyakazi wa jinsia nyingine kama huna ujasiri wa kuutambulisha kwa
mwenzi wako au wafanyakazi wengine.
Kutafuta hisani
Elizabeth (si jina lake halisi) ni mwalimu wa shule ya sekondari.
Anakiri alishakuwa na uhusiano wa kimapenzi na Mkuu wa Shule. ‘Nilijua kabisa
ninachokifanya si sahihi. Nilikuwa na mume na mtoto mmoja. Sikufikiria kabisa
matokeo yake,’ anaeleza.
‘Nakumbuka ilianza (mapenzi) wakati niko kwenye wakati mgumu
kiuchumi. Mambo yalikuwa magumu sana. Sikuwa napata nafasi za kwenda kwenye
kazi maalum (kusaisha mitihani) […] Sasa nadhani Mkuu (wa Shule) alijua
nahitaji sana hela. Ndio ikawa hivyo.’
Mazingira ya Elizabeth yanawapata wanawake wengi wanaohitaji
kupata upendeleo usiofuata utaratibu. Msichana anayetafuta kazi anaweza kuingia
kwenye vishawishi vya kuanzisha uhusiano na mtu anayeweza kumwezesha kupata
kazi. Pia wafanyakazi wanaotaka kupata fursa zisizopatikana kirahisi nao
wanaweza kushawishika kuwa na uhusiano na wakubwa kazini.
Mwanzoni inaweza kuonekana kama bahati kuwa na uhusiano wa
kimapenzi na mtu mwenye ushawishi kazini, mtu anayeongoza vikao, ambaye maoni
yake yanaweza kuamua hatima ya ajira yako. Lakini, siku zote, uhusiano wa namna
hii hukufanya uwe mtumwa. Utalazimika kulinda kazi yako kwa kuendeleza uhusiano
wa kimapenzi ambao baadae utagundua haukunufaishi kama unavyofikiri.
Tafuta kuonekana kazini kwa kufanya kazi kwa bidii. Ikiwa kuna
vikwazo, vichukulie kama sehemu ya changamoto bila kulazimika kujidhalilisha
kama namna ya kutafuta ufumbuzi.
Kutokuwa na mipaka
Dorcas anasimulia namna alivyozoeana na Johnson zaidi ya ofisini.
‘Kuna nyakati tulikuwa tunalazimika kwenda kufanya kazi nyumbani. Tulishazoeana
sana mpaka maneno yakaanza kuzuka tunatoka wote ingawa haikuwa hivyo. Basi
tumekunywa pombe kidogo pale kwake ikawa ndio kweli.’
Ingawa si jambo baya kuendeleza ukaribu na mfanyakazi mwenzako nje
ya ofisi, kuna uwezekano wa mazoea hayo kutengeneza vishawishi. Dorcas
anaeleza, ‘Mwanzoni kweli nilijiaminisha ningeweza kujizuia. Lakini ndio hivyo
shetani akanipitia tukawa tunakutana mara kwa mara.’ Kutokuwa na mipaka ya kazi
inaweza kuwa tatizo. Mazoea ya kufanya kazi na mtu huyo huyo nje ya ofisi
yanapoachwa yakomae, huweza kutengeneza hisia zisizotarajiwa.
Morice, Mhasibu wa Shirika moja la Umma aliyejikuta kwenye mapenzi
na mfanyakazi mwenzake alikubaliana na tahadhari ya Dorcas. ‘Ilianza kwenye
safari za kikazi. Hatukuwa tunaenda wawili. Lakini si unajua ule ukaribu mkiwa
nje na ofisi? Utani wa hapa na pale […] mzee nikaanza kumpenda.’
Mume wa Dorcas aligundua uhusiano huo kupitia wafanyakazi wengine
wa ofisi. Uhusiano wa ofisini umeihamishia ndoa yake jangwani. Ofisini, hivi
sasa Dorcas hana amani shauri ya maneno yanayosikika kwenye vikao vya chai na
koridoni. Utendaji wake kazini umeathirika na sasa anafikiria namna ya kuondoka
hapo alipo kutafuta kazi mahali pengine. Kufahamika kwa uhusiano wa kimapenzi
usiotarajiwa, ni moja wapo ya sababu zinazowafanya watu wengi wafanye maamuzi
ya kuacha kazi.
0 Response to " Mazingira Yanayoweza Kuanzisha Mapenzi Yasiyotarajiwa Kazini"
Post a Comment