MAPENZI YA MTANDAONI YALIVYOLETA MAUAJI...
MAPENZI YA MTANDAONI YALIVYOLETA MAUAJI...
Duniani humu kuna matukio yanayotokea, ambayo ukisimuliwa unaweza ukadhani ni sehemu ya tunzi za waandishi mahiri. Lakini, ni matukio ya kweli kabisa yanayobaki kushangaza maelfu ya watu wanaoyaona ama kuyasikia kama si kuyasoma.
Mapenzi ni moja ya vitu vinavyosababisha matukio haya ya ajabu mbele ya milango yetu ya fahamu. Mikasa yake huwa inaifanya dunia ihoji utimamu wa akili za wahusika. Ninakuletea kisa hiki cha mapenzi ya mtandaoni ambacho kimeniacha hoi bin taabani garagara mauti!
Ungana nami sasa uyashuhudie ya walimwengu!
YALIKOANZIA…..
Mwaka 2005. Kipindi hicho kwenye mtandao unaoitwa Pogo, kulikuwa na chatroom ambayo vijana walijumuika kuchat kwa pamoja na wengine kwenda faragha (Inbox) kuendeleza maongezi yao na kujenga mahusiano zaidi ya kirafiki au kimapenzi. Kwa wale walioanza mambo ya mitandao mapema, mtakumbuka DarHotwire Chatroom ilivyokuwa.
Basi bwana, kama ilivyo kawaida kwenye hizi Chatroom mitandaoni watu hutumia majina feki. Huyu atajiita Mbuyumaziwa yule atajiita Cuteangelbarbie na kadhalika na kadhalika. Na ndivyo ilivyokuwa katika mtandao wa Pogo pia. Mtandao uliojulikana kuwa unatumiwa zaidi na vijana wadogo kiumri.
May, 2005.
Siku hii, Thomas Montgomery aliyekuwa na umri wa miaka 46 wakati huo, Mume wa Cindy Montgomery na baba wa watoto wawili, alijiunga Pogo Chatroom akitumia jina la bandia la MarineSniper.
Kwa vile alitumia picha yake iliyomuonyesha kuwa ni mtu mzima. Akapokea meseji toka kwa mtumiaji mwingine wa Pogo chatroom aliyekuwa anatumia jina la Talhotblond kuwa alikuwa amekosea room kwa kuwa chatroom hiyo ilikuwa ya vijana wadogo.
Hapo hapo, Tom aliamua kudanganya kuwa alikuwa ameingia chatroom ile kwa account ya baba yake na kwamba jina lake halisi alikuwa anaitwa Tommy na umri wake ni miaka 18. Akaendelea kudanganya kuwa alikuwa mwanajeshi wa majini(Marine) na kwamba ndiyo kwanza alikuwa ametoka jeshini Iraq.
Katika utetezi wake wakati akihojiwa, Thomas alisema alidanganya hivyo kwa kujiaminisha kuwa zilikuwa ni chats za mtandaoni tu na kwamba kamwe isingetokea wakaonana uso kwa uso au kufahamiana zaidi.
Alijidanganya!
Walikuwa wakichat public kwenye ile chatroom ya pamoja ambayo kila mtu aliongea kivyake na wengine kutaniana hapo hapo na kadhalika.
Ila taratibu wakahamia inbox ambako huyo Talhotbond alimwambia yeye anaitwa Jessi, ni msichana wa miaka 18 pia na anasoma high School hapo West Virginia anakoishi.
Akatuma picha zake kwenda kwa Thomas ambaye anakiri zilikuwa picha za kuvutia mno kimapenzi na kushawishi.
Jessi (Talhotbond) akamuomba na yeye Tommy (MarineSniper) amtumie picha pia. Sasa ili kwenda sambamba na uongo wake ikabidi Tommy atume picha za miaka 30 iliyopita alipokuwa mwanajeshi kiukweli. Ambapo wakati huo alishaachana na mambo ya jeshi na alikuwa mfanyakazi kiwandani.
Kiutani utani tu, wakajikuta wanaanza kuflirt, muelekeo wa mazungumzo yao ulikuwa wa kimapenzi na sio kirafiki tena. Walizungumza kila siku, kila mara. Hali hii ilimfanya Tommy baba mtu mzima mwenye mke wake, ajione kama kijana kila mara alipokuwa akizungumza na Jessi.
Alijihisi mwenye furaha kubwa mno katika mahusiano yake ya mtandaoni kuliko yale aliyokuwa nayo katika maisha halisi. Alipata faraja mno.
Jessi alimfanya ajisikie anapendwa, anajaliwa kila mara alipokuwa anamkumbusha namna anavyompenda na kuwa atampenda milele zote. Waliandikiana vitu vya kimahaba na kuamshiana ashki za mapenzi.
Thomas akakiri kuwa ilimfanya wakati mwingine ajisikie vibaya na mwenye hatia lakini raha, kujaliwa na amani ya moyo aliyokuwa anapewa na Jessi vilimfanya ashindwe kukatiza mahusiano yao hata pale alipoona alipaswa kuacha kufanya alichokuwa anafanya.
Alizidiwa na hisia za kutaka kuzungumza na Jessi kila siku, kila wakati tena kwa muda mrefu!
Walitumiana zawadi, na Thomas ndiye aliyetuma zawadi kila mara.
Katika kupekua wakati wa uchunguzi, walikuta Note ya Thomas aliyojiandikia mwenyewe kuwa ‘Jan 2, 2006 yeye Tom Montgomery, miaka 46, alikuwa ametoweka na sasa alikuwepo kijana wa miaka 18, mwanajeshi wa jeshi la majini, mwenye uso unaofanana na Msanii Harrison Ford.’
Hii ilionyesha ni kiasi gani uongo alioutunga mwenyewe ulimkaa kichwani barabara na aliufurahia. Alimsimulia Jessi matukio ya kijeshi yaliyotokea uko Fallujah na Jessi naye alimtumia picha zake alizovaa bikini huku akiziweka chapa ya ‘Tommy and Jessi forever’.
BWANA LIKAINGIA RUBA….
March, 2006
Mapenzi yao matamu, yaliyojaa mahaba ya kufa mtu yakaingia dosari ghafla! Mke wa Tom alizifuma picha za Jessi na chats zake na mumewe. Kwa hasira aliamua kumtumia Jessi picha halisi ya Tom akiwa na familia yake.
Akamwambia
‘Ngoja nikutambulishe kwa watu hawa huyo wa katikati ni mume wangu tangu 1989, ana miaka 46…’
Mke akaufunua uongo wote wa Tom na kilichotokea, Jessi alionekana kuogopa kwa mujibu wa maelezo ya Tom mwenyewe. Alimjia juu na kumkasirikia kwa kumdanganya huku akimwambia anamchukia kupita maelezo. Tom akaomba msamaha sana na akaendelea kukiri kuwa anampenda kiukweli kabisa toka moyoni.
Kwa kuwa identity ya Tom ilishakuwa wazi, Jessi akagundua sehemu aliyokuwa anafanyia kazi Tom kulikuwa na mfanyakazi mwenzake aitwaye Brian Berret, kijana wa miaka 22 tu, ambaye katika chatroom alikuwa anatumia jina la Beefcake.
Jessi akamfuata chemba Brian na kumueleza kila kitu na wakajikuta wanakuwa karibu, Brian alikuwa kama mfariji sababu Jessi alionyesha kuumia sana.
Wakati wote huu si Tom wala Brian aliyewahi kuonana na Jessi na wala si Jessi aliyewahi kuonana na wanaume hawa wawili. Walitumiana tu picha na kupigiana simu!
Ukaribu wa Jessi na Brian ulianza kuonekana kwenye chatroom ya public ambayo Tom alikuwa anaiona. Jessi alifanya kusudi kabisa kuonyeshea kwa Tom kuwa sasa alikuwa na Brian na hapo hapo alimsema katika Chatroom kuwa ni mbaba wa miaka 47 na sio kijana hivyo kumfanya asithubutu kuchangia chochote akihofia kushambuliwa na wanachatroom waliokuwa wakimdhihaki.
Yote yaliyokuwa yanaendelea aliyaona, aliumia si kwa kuumbuliwa ila kwa kuachwa na Jessi na namna alivyoonyesha kuwa mapenzini na Beefcake ambaye sasa aligundua kumbe ni Brian mfanyakazi mwenzake!! Aligundua sababu Brian aliwasimulia watu kazini alichoelezwa na Jessi.
Alijicontrol alivyoweza na akajaribu kuendelea na maisha bila kumtafuta Jessi. Lakini, Jessi mwenyewe ndiye aliyeanza tena kujileta kwa Tom. Akidai amemmiss sana na kumuuliza kama amemmiss pia. Tom akajibu hisia zake bado zilikuwa kwake. Na moyo wake ulikuwa unaumia Jessi alipokuwa anamuita Tommy kama zamani, alitamani kweli angekuwa na miaka 19 kama alivyodanganya.
Jessi akamwambia anampenda hata hivyo alivyo! Na hii ilikuwa kama kumpa tena teja dawa za kulevya! Ilikuwa furaha kubwa mno kwa Tom, kuwa sasa hakuwa na sababu ya kujificha kwa kuwa alikuwa anapendwa na umri wake huo huo wa miaka 47 sasa! Alijawa na furaha mno na akajiona kama mtu mwenye bahati duniani.
Ingawa alikuwa anajificha mkewe asimshtukie tena, lakini alikuwa na amani zaidi. Na aliutumia muda mwingi kuzungumza na Jessi ambaye alimfanya Tom awe huru mno kuzungumza naye hata mambo binafsi, ni kama vile Jessi alikuwa egemeo lake kuu duniani na Tom alimuona Jessi kama mwanamke pekee anayemuelewa na kumsikiliza, ukichanganya na uzuri aliouona kwenye picha, Tom alidata!
Kumbe wakati huo Jessi alikuwa ameachana na Brian kwa muda na waliporudiana tena Jessi akamwambia Tom kuwa mapenzi yao yafike mwisho.
Alimvuruga mno, vibaya sana!
Obsession ikaanza kugeuka kuwa wivu, ukichanganya na maumivu, Tom alijiona kama mtu aliyesalitiwa vibaya. Maumivu yake yalizidi alipopata habari kuwa Jessi alikuwa amemuacha ili kurudiana na Brian ambaye alikuwa anapanga kuonana na Jessi uso kwa uso kwa mara ya kwanza.
Tom aliumia sana!
Mara moja alimtumia Jessi meseji kuwa Brian atalipa maumivu yake kwa damu hata hivyo alijirudi na kuomba radhi akimbembeleza Jessi asimuache.
Na alipoona Jessi hamuelewi Tom aliwasha gari akielekea West Virginia pengine akitaka kuwahi kumuona Jessi kabla ya Brian, lakini Jessi alimtumia ujumbe wa kumtaka asije kwake kabisa.
MAUAJI….
September 15, 2006
Brian Barret akiwa anatoka kazini, kwenye eneo la maegesho alipigwa risasi tatu na kufariki papo hapo.
Polisi walisema risasi zilizomuua Brian zilikuwa zimepigwa toka katika bunduki ya kijeshi. Polisi walianza uchunguzi na ndipo wafanyakazi wenza waliokuwa karibu na Brian walisimulia mkasa wa Brian kumpenda mwanamke wa mtandaoni aitwaye Jessi, aliyekuwa anapendwa na mfanyakazi mwenzao aitwaye Thomas Montgomery, na kwamba Brian alikuwa njiani kwenda kuonana uso kwa uso na huyo Jessi.
Polisi kwa kuhofia usalama wa Jessi, waliamua kupitia maongezi ya Brian na Jessi kwenye kompyuta na kutafuta pa kuanzia uchunguzi wao ikiwemo sehemu ya kumpata Jessi ili wamuweke mbali na Thomas ambaye alikuwa mtuhumiwa namba moja.
KITUKO CHA MWAKA….
Polisi walipofika nyumbani kwa akina Jessi walimkuta mama yake Mary Shieler aliyekuwa na miaka 45, na kumueleza kuwa kulikuwa na mauaji yaliyofanyika sababu ya binti yake na walikuwa wanaohofia muuaji angeweza kumdhuru hata Jessi, hivyo walikuwa wanamtafuta Jessi.
Kwanza alishtuka mno kusikia kuna mauaji ni kama hakuamini!
Mama wa watu akaangua kilio!
Ndipo sasa akaanza kujieleza kuwa, Jessi aliyekuwa anawasiliana na hawa wanaume ni yeye mwenyewe Mary na sio binti yake ambaye ni kweli anaitwa Jessi.
Akakiri Jessi alikuwa hajui chochote kuhusu Brian wala Thomas na kwamba alikuwa akitumia picha za binti yake kwenye hizo chatrooms. Hakujua atasababisha mauaji!
Polisi wakachoka!
Binti akatafutwa ni kweli hakuwa anajua chochote kuhusu Brian na Thomas. Na alishtuka zaidi kusikia mama yake alikuwa akitumia picha zake kutumia wanaume. Akakumbuka mara kadhaa alikuwa akimrekodi lakini hakujua mama yake alikuwa anafanyia mambo ya ovyo picha na video zake.
Kijana wa watu Brian Barret, mwanafunzi wa chuo na mfanyakazi hapo kiwandani akawa ameuawa hivi hivi sababu ya mapenzi ya mtandaoni. Kumbe hata huyo Jessi sio binti, ni mmama wa miaka 45 aliyeamua kuchezea akili za wanaume mitandaoni. Brian ameacha huzuni kubwa kwa wazazi, ndugu, jamaa na marafiki!
Thomas Montgomery alihukumiwa kifungo cha miaka 20 anatarajia kuachiwa huru mwaka 2026. Yuko gerezani mpaka sasa. Aliacha familia yake ikiwa haiamini baba yao mtu mzima mwenye mke, alipenda mtu hadi kufikia hatua ya kuua!
Jessi Shieler, Jessi halisi. Alikata mawasiliano na mama yake kabisaaa. Hakutaka tena kuwasiliana na mama yake wala kuwa naye karibu baada ya kugundua alichofanya.
Mary Shieler, alikosea kijamii ila kisheria hakuonekana kuwa na kosa lolote lile. Hivyo yuko huru lakini mumewe alimtaliki mara moja baada ya siri yake kufichuka na pia binti yake amemtenga mpaka sasa. Iligundulika kuwa mbali na Brian na Thomas, Mary alikuwa akiwachezea akili wanaume wengine wawili kwa kutumia jina la binti yake na picha za binti yake.
Mara moja katika mahojiano, Mary alisema, hakutarajia uongo wake ungesababisha mauaji, alijua ni michezo tu ya mitandaoni basi, lakini mauaji yalipotokea hakuamini mambo yamefikia hapo. Amepoteza binti, amepoteza mume, kwa kipindi kirefu aliishi akijificha sababu ya kutapakaa kwa habari. Anautumia muda wake mwingi kufanya kazi za kijamii.
Natumaini umejifunza kitu katika hii habari!.... mapenzi huwa yana nguvu sana yanapozama moyoni! Usichezee moyo wa mtu, usichezee akili ya mtu iwe mtandaoni au wapi. Mapenzi yanazaa obsession inayopelekea matukio ya ajabu sana!
Mapenzi ni hisia, pasipo hata kumuona mtu live unaweza ukajikuta unafall mzima mzima, ni vile ambavyo mtu anafanikiwa kuichota akili yako na moyo wako! na watu wa nje tunabaki kuulizana utimamu wa akili yako.
kuna movie ya hili tukio inaitwa TALHOTBLOND ilitoka 2009.
TAMATI!!
Kwa msaada wa mitandao mbalimbali
Imetafsiriwa na kuandikwa na Laura Pettie
0 Response to "MAPENZI YA MTANDAONI YALIVYOLETA MAUAJI..."
Post a Comment