JINSI YA KUKOMESHA MIZOZO NYUMBANI - Bongo Loves

JINSI YA KUKOMESHA MIZOZO NYUMBANI

UFANYE  nini ikiwa inaonekana kwamba mizozo katika familia yako haiishi? Huenda mizozo hiyo imekuwa mibaya zaidi na inatokea mara nyingi zaidi. Labda hata hujui chanzo cha ugomvi huo. Lakini bado mnapendana na hamtaki kuumizana.
Ni muhimu kukumbuka kwamba kwa kuwa tu mna maoni yanayotofautiana, haimaanishi kwamba familia yenu inasambaratika. Kinachoamua ikiwa nyumba yenu itakuwa na amani au la, si ugomvi wenyewe bali ni jinsi mnavyoushughulikia. Fikiria hatua zifuatazo zinazoweza kuwasaidia kukomesha mizozo.
Acha kulipiza kisasi.
Ili kuwe na mabishano, lazima kuwe na watu wawili wanaozungumza. Lakini mmoja anaponyamaza na kusikiliza badala ya kuzungumza, mabishano huisha. Kwa hiyo, epuka kumjibu mwenzako unapokasirishwa. Dumisha heshima yako kwa kujizuia. Kumbuka, kuwa na amani katika familia ni muhimu zaidi kuliko kushinda mabishano.
Elewa hisia za wengine katika familia.
Kumsikiliza mwenzako kwanza kwa makini ukiwa na hisia-mwenzi bila kumkatiza au kumhukumu kunaweza kutuliza hasira na kudumisha amani. Badala ya kumshuku mwenzako, tambua hisia zake. Usifikiri ana nia mbaya wakati amekosea tu kwa sababu ya kutokamilika. Huenda akasema maneno yenye kuudhi bila kufikiri au kwa sababu ameumizwa hisia na si kwa sababu ana kinyongo au analipiza kisasi.
Jipatie nafasi ya kutulia.
Ukikasirika, huenda ikafaa uondoke kwa busara ili utulie kidogo. Unaweza kwenda kwenye chumba kingine au ukatembee hadi utakapokuwa sawa. Kufanya hivyo si sawa na kumnyamazia mwenzako. Badala yake, huenda ni nafasi nzuri ya kusali ili Mungu akupe subira, ufahamu, na uelewaji.
Fikiria kwa makini ni nini kinachohitaji kusemwa na jinsi ya kukisema.
Hakuna faida ya kutafuta maneno ya kujibizana na mwenzako. Badala yake, jaribu kusema jambo litakalotuliza hisia zilizoumizwa za mpendwa wako. Na badala ya kumwamulia mwenzako hisia zake, mwombe ajieleze na umshukuru kwa kukusaidia kuelewa hisia zake.
Zungumza kwa sauti ya chini na kwa njia inayoonyesha unatafuta mapatano.
Mtu mmoja katika familia anapokosa subira anaweza kuamsha hasira ya mwenzake. Epuka kejeli, matusi, au kuzungumza kwa sauti ya juu, hata ikiwa unahisi umekosewa. Epuka kuwalaumu wengine kwa kusema mambo kama vile “Wewe hunijali” au “Wewe hunisikilizi kamwe.” Badala yake, mweleze mwenzi wako kwa utulivu jinsi ambavyo mwenendo wake ulivyokuathiri (“Ninaumia unapo . . . ”). Hupaswi kamwe kumsukuma mwenzako, kumpiga kofi, teke, au kumtendea kwa jeuri ya aina nyingine. Pia, hupaswi kumtukana, kumdhihaki, au kumtisha mwenzi wako.
Omba msamaha na eleze nini utafanya ili kurekebisha hali.
Usiache hisia zisizofaa zikufanye usahau kwamba lengo lako kuu ni kufanya amani. Kumbuka kwamba hamfaidiki mkilumbana. Lakini mkifanya amani, nyote wawili mnafaidika. Kwa hiyo, kubali kosa lako. Hata ikiwa unasadiki kwamba hujakosea, unaweza kuomba msamaha kwa sababu ya kukasirika, kwa kutenda kwa njia isiyofaa, au kwa kumkasirisha mwenzako bila kukusudia. Kudumisha amani kati yenu ni muhimu kuliko kushinda bishano. Na ukiombwa msamaha, uwe tayari kusamehe.
Chanzo: Mashahidi wa Yehova
USISAHAU KUSHARE NA KUCOMMENT APPLICATION YETU YA KONA YA MAHABA❤️😘😍 https://play.google.com/store/apps/details?id=tz.konayamahaba.app&hl=en

0 Response to "JINSI YA KUKOMESHA MIZOZO NYUMBANI"

Post a Comment