Ukitaka Mwenzako Akuamini, Jifunze Kutanguliza Mahitaji Yake - Bongo Loves

Ukitaka Mwenzako Akuamini, Jifunze Kutanguliza Mahitaji Yake

 
 Image result for mahaba
Kwa mujibu wa Maslow, unahitaji ‘kushibisha’ ule ubinafsi unaoishi ndani yako kwanza ili upate nguvu za kupanda ngazi ya juu kabisa ya ustawi wa mwanadamu. Maslow anasema wakati huo ‘unaposhibisha’ ubinafsi wako, muda mwingi utautumia ‘kupambana na hali yako’ kuliko kujali ustawi wa watu wengine. Utakuwa na marafiki unaowatumia ‘kushibisha’ ubinafsi wako. Utatamani kupendwa kuliko kupenda. Utatarajia kupewa kuliko kutoa.
Hata hivyo, Maslow anasema, kadri njaa hiyo ya kukidhi mahitaji yako binafsi inavyoshibishwa, ndivyo unavyopanda ngazi kuanza kujali mahitaji ya watu wengine. Katika hatua hii, Maslow anasema, mwanadamu hujiona anacho kitu cha kumpa mwingine. Furaha yake huanza kutegemea namna anavyoweza kugusa maisha ya wengine kuliko anavyonufaika kibinafsi. Ikiwa hivyo, kwa mujibu wa Maslow, basi unakuwa umefikia hatua ya juu kabisa ya kupevuka kama binadamu aliyestawi na kufanikiwa.
Urafiki kati ya watu wawili waliofikia hatua hii ya ustawi wa nafsi una nafasi kubwa ya kuleta utoshelevu mkubwa kwa sababu kuu mbili. Kwanza, kila mmoja anakuwa na nguvu ya kuvaa viatu vya mwenzake akitaka kuelewa mahitaji yake. Mazungumzo yao, kwa mfano, hujaa usikivu na uzingativu kuliko kuongea na kutaka kusikika. 

Mnasihi maarufu Carl Rogers aliuita uwezo huu, empathetic understanding, yaani kuvaa viatu vya mwenzako ili kuelewa kile anachojaribu kukisema. Hii ndiyo sifa ya mtu anayetanguliza mahitaji ya mwenzake. Hata pale mtu huyu anapokuwa hakubaliani na mtu, bado ni rahisi kwake kuvumilia. Uvumilivu ni tabia ya mtu anayetambua upande wa mwenzake.
Niliwahi kukutana na Evans (sio jina lake halisi) aliyekuwa na mgogoro na mke wake.  Evans alikuwa na shida ya mawasiliano na mke wake aliyekuwa amezira kwa hasira kwa majuma kadhaa. Mara nyingi walipojaribu kuzungumza, Evans aliniambia, waliishia kugombana. Ukuta mkubwa wa mawasiliano ulikuwa umejengeka kati ya Evans na mke wake.
Katika mazungumzo yetu, niligundua Evans alikuwa na tatizo la kutokusikiliza. Muda mwingi katika mazungumzo yetu, Evans alishika shika simu yake kufuatilia kilichokuwa kinaendelea kwenye mitandao ya kijamii. Wakati mwingine alipiga simu bila hata kuomba radhi. Hakuwa na utulivu. Nilihisi hiyo ndiyo tabia yake hata anapokuwa nyumbani. Nilimwomba kukutana na mke wake pia kama sehemu ya kutafuta ufumbuzi. Alinikubalia.
Mke wake alithibitisha hisia zangu. Alalamika namna Evans alivyo mwanaume mbinafsi asiyejitambua. Alitoa mfano kuwa mara zote walipozungumza, Evans alishikilia msimamo wake. Evas hakupenda kusikiliza upande wa mke wake. Wakati mwingine alifanya maamuzi yanayopendelea upande wake bila kuzingatia mke wake alifikiri nini. Ilikuwa dhahiri mke wake alikuwa amechoshwa na tabia ya Evans kujitanguliza mwenyewe.
Evans alihitaji kujifunza tabia mpya ya kumtanguliza mke wake. Evans alihitaji kujifunza kuwa msikivu na kuvaa viatu vya mkewe. Tulifanya zoezi la kusikiliza kwa uzingativu. Tulijifunza umuhimu wa kuacha kutumia simu, tabia ya kuangalia wapita njia, kupiga miayo, na kujenga tabia ya kufuatilia anachokisema mwingine kwa vitendo. Haikuwa kazi rahisi lakini hatimaye Evans alielewa. Evans alijifunza namna tabia yake ya kujitanguliza ilivyochangia tatizo kinyume na mawazo aliyokuwa nayo awali.
Evans alirudi nyumbani kufanyia kazi tuliyojifunza. Alianza kujifunza ‘kumpa masikio’ mke wake na kuelewa mtazamo wake. Evans alianza kutanguliza hisia za mke wake badala ya kuweka mbele hisia zake. Haikuwa rahisi mwanzoni. Lakini aliposimamia tabia hiyo mpya kwa muda, taratibu mke wake alianza kumwamini. Moyo wake ukaanza kufunguka kwa Evans. Nilipokutana na Evans majuma kadhaa baadae aliniambia, “Kumbe kumtanguliza (mke wangu) kumenisaidia kupata nilichokitaka.” Evans aliaminika kwa sababu alijifunza kumtanguliza mke wake.
Hiki ndicho ninachomaanisha ninaposema ndoa bora hujengwa kwa uwezo wa kumtanguliza mwenzako. Ingawa kwa haraka haraka inaweza kuonekana ni utumwa wa namna fulani, lakini mwisho wa siku, unapomtanguliza mwenzako, wewe ndiye unayenufaika kwa kumfanya mwenzako naye asukumwe kufikiria mahitaji yako.
Evans angeendelea kusisitiza jinsi alivyo sahihi kwa mipango na tabia yake badala ya kufikiri mke wake naye anawaza nini, asingeweza kubomoa ukuta wa mawasiliano uliokuwa umejengeka kati yao. Kwa maana nyingine, kutanguliza mahitaji yake kungemnyima hitaji lake la kuwa karibu na mke wake.

Nimalizie kwa kukuuliza, mara ngapi umeshindwa kujua mwenzako anahitaji nini kwa sababu muda wote umekuwa ukitanguliza kile unachokitaka? Je, kwa kutanguliza matakwa yako, umekuwa ukijanga uhusiano wako na mwenzako? Pengine unahitaji kujifunza kumtanguliza mwenzako. Kwa kufanya hivyo mwenzako atakuamini kama ilivyotokea kwa Evans.

0 Response to "Ukitaka Mwenzako Akuamini, Jifunze Kutanguliza Mahitaji Yake "

Post a Comment