Mazingira Yanayoweza Kuanzisha Mapenzi Yasiyotarajiwa Kazini
Dorcas, msichana wa miaka 30 anayefanya kazi kama Afisa Mikopo kwenye benki moja mjini, hakuwahi kufikiri ingetokea siku moja ‘achepuke’ kimapenzi na Johnson ambaye ni mfanyakazi mwenzake. Miaka mitatu iliyopita wakati anaanza kazi kwenye benki hiyo, Dorcas alikuwa na msimamo thabiti na aliheshimu ndoa yake.
Ingawa alifanya kazi kwa karibu na Johnson, Dorcas hakumchukulia kama mtu mwenye sifa stahiki za kumvutia kimapenzi. Kilichotokea mwaka mmoja baadae, kwa mujibu wa Dorcas, hakieleweki. Dorcas si tu amejikuta kwenye penzi zito na Johnson, lakini amejikuta akichafua sifa yake na kuhatarisha kazi yake.
Ingawa mapenzi ofisini huwaathiri wahusika wote wawili, mara nyingi mwathirika mkubwa huwa ni mwanamke. Kisaikolojia, mwanamke huchukulia mapenzi kwa hisia na uzito zaidi kuliko mwanaume. Pia inapotokea wawili hao wamebainika, jamii yetu humwadhibu mwanamke kwa maneno na hisia kuliko mwanaume.
Sote tunafahamu hatari ya mapenzi kazini. Mbali na kupoteza kazi ukiingia pasipoingilika, unaweza kuharibu sifa yako, ukapoteza furaha ya kazi na hata kuvuruga ndoa/mahusiano uliyonayo. Jambo la kujiuliza, hata hivyo, ni kwa nini watu ambao awali wasingedhani wangejikuta kwenye lindi la mapenzi na wasiyemtarajia, hujikuta katika mazingira ambayo hawawezi tena kujizuia?
Mazoea ya kikazi
Wafanyakazi wengi hujikuta wakijiwa na hisia za kimapenzi na wafanyakazi wenzao kwa sababu ya kutumia muda mwingi pamoja. Dorcas anaeleza jambo hili vizuri. ‘Hata sijui ilikuwaje. Sikujua kinachoendelea hata. Tulikuwa tunafanya kazi pamoja kwa muda mrefu. Nikaanza kupenda kazi yake. Nikaanza kuvutiwa na bidii yake kazini. Basi nikajikuta nampenda.’
Ofisi inaweza kuwa bustani ya mapenzi. Kufanya kazi kwa karibu na kwa muda mrefu pamoja kunaweza kuzalisha hisia zisizotarajiwa kama ilivyotokea kwa Dorcas.
‘Tulifanya kazi kwa karibu sana,’ anasimulia. ‘Unajua kipindi hicho sikuwa nafahamu vizuri kazi. Johnson ndio akawa msaada wangu pale ofisini. Wakati mwingine tulikaa mpaka usiku tukikimbizana na deadline (saa ya kukabidhi kazi)…kidogo kidogo nikaanza kumpenda.’
Pamoja na umuhimu wa kufanya kazi kwa ukaribu na wenzako, ni muhimu kujiwekea misimamo itakayokulinda. Epuka kuweka mazingira ya urafiki wa karibu na wafanyakazi wa jinsia nyingine kama huna ujasiri wa kuutambulisha kwa mwenzi wako au wafanyakazi wengine.
Kutafuta hisani
Elizabeth (si jina lake halisi) ni mwalimu wa shule ya sekondari. Anakiri alishakuwa na uhusiano wa kimapenzi na Mkuu wa Shule. ‘Nilijua kabisa ninachokifanya si sahihi. Nilikuwa na mume na mtoto mmoja. Sikufikiria kabisa matokeo yake,’ anaeleza.
‘Nakumbuka ilianza (mapenzi) wakati niko kwenye wakati mgumu kiuchumi. Mambo yalikuwa magumu sana. Sikuwa napata nafasi za kwenda kwenye kazi maalum (kusaisha mitihani) […] Sasa nadhani Mkuu (wa Shule) alijua nahitaji sana hela. Ndio ikawa hivyo.’
Mazingira ya Elizabeth yanawapata wanawake wengi wanaohitaji kupata upendeleo usiofuata utaratibu. Msichana anayetafuta kazi anaweza kuingia kwenye vishawishi vya kuanzisha uhusiano na mtu anayeweza kumwezesha kupata kazi. Pia wafanyakazi wanaotaka kupata fursa zisizopatikana kirahisi nao wanaweza kushawishika kuwa na uhusiano na wakubwa kazini.
Mwanzoni inaweza kuonekana kama bahati kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mtu mwenye ushawishi kazini, mtu anayeongoza vikao, ambaye maoni yake yanaweza kuamua hatima ya ajira yako. Lakini, siku zote, uhusiano wa namna hii hukufanya uwe mtumwa. Utalazimika kulinda kazi yako kwa kuendeleza uhusiano wa kimapenzi ambao baadae utagundua haukunufaishi kama unavyofikiri.
Tafuta kuonekana kazini kwa kufanya kazi kwa bidii. Ikiwa kuna vikwazo, vichukulie kama sehemu ya changamoto bila kulazimika kujidhalilisha kama namna ya kutafuta ufumbuzi.
Kutokuwa na mipaka
Dorcas anasimulia namna alivyozoeana na Johnson zaidi ya ofisini. ‘Kuna nyakati tulikuwa tunalazimika kwenda kufanya kazi nyumbani. Tulishazoeana sana mpaka maneno yakaanza kuzuka tunatoka wote ingawa haikuwa hivyo. Basi tumekunywa pombe kidogo pale kwake ikawa ndio kweli.’
Ingawa si jambo baya kuendeleza ukaribu na mfanyakazi mwenzako nje ya ofisi, kuna uwezekano wa mazoea hayo kutengeneza vishawishi. Dorcas anaeleza, ‘Mwanzoni kweli nilijiaminisha ningeweza kujizuia. Lakini ndio hivyo shetani akanipitia tukawa tunakutana mara kwa mara.’ Kutokuwa na mipaka ya kazi inaweza kuwa tatizo. Mazoea ya kufanya kazi na mtu huyo huyo nje ya ofisi yanapoachwa yakomae, huweza kutengeneza hisia zisizotarajiwa.
Morice, Mhasibu wa Shirika moja la Umma aliyejikuta kwenye mapenzi na mfanyakazi mwenzake alikubaliana na tahadhari ya Dorcas. ‘Ilianza kwenye safari za kikazi. Hatukuwa tunaenda wawili. Lakini si unajua ule ukaribu mkiwa nje na ofisi? Utani wa hapa na pale […] mzee nikaanza kumpenda.’
Mume wa Dorcas aligundua uhusiano huo kupitia wafanyakazi wengine wa ofisi. Uhusiano wa ofisini umeihamishia ndoa yake jangwani. Ofisini, hivi sasa Dorcas hana amani shauri ya maneno yanayosikika kwenye vikao vya chai na koridoni. Utendaji wake kazini umeathirika na sasa anafikiria namna ya kuondoka hapo alipo kutafuta kazi mahali pengine. Kufahamika kwa uhusiano wa kimapenzi usiotarajiwa, ni moja wapo ya sababu zinazowafanya watu wengi wafanye maamuzi ya kuacha kazi.
Ingawa ni kweli ofisi inaweza kukukutanisha na mwenzi wako wa maisha, kama inavyotokea kwa baadhi ya watu, ni muhimu mfanyakazi kuifanya ofisi ibaki kuwa eneo la kazi. Epuka kulea ukaribu unaoweza kuharibu sifa yako na kuhatarisha kibarua chako.
0 Response to "Mazingira Yanayoweza Kuanzisha Mapenzi Yasiyotarajiwa Kazini "
Post a Comment