FANYA HAYA KWA FAIDA YA MAPENZI YAKO
Kupendana kwa dhati ni nguzo imara inayofanya mapenzi baina ya wapendanao yaweze kuwa imara na madhubuti. Wanaopendana kwa dhati wanasikilizana, kuhesimiana na kila mmoja kuwa na hamu na shauku na mwenzake.
Katika mapenzi hivyo ni vitu muhimu sana. Ili mapenzi yaweze kustawi heshima inabidi iwepo baina ya wahusika. Ili kila mmoja aweze kuwa na furaha na faraja katika mahusiano inabidi miongoni mwao kuwepo na hamu na shauku. Mmoja akikosa hali hii mapenzi hukosa ladha. Si ajabu kuona mwingine akianza kuhisi anajipendekeza kwa mwnenzake au kuona akikosa raha kabisa ndani ya mahusiano hayo.
Wewe uko vipi kwa mpenzi wako?
Je, unampa sababu ya kwenda kifua mbele kwa marafiki zake na kusema anamtu anayempenda kwa dhati? Umempa jeuri hiyo mwenzako?Au ndiyo vile kila siku unamfanya asitamani kuwepo mapenzi katika dunia!
Unafanya ajivunie kuwa katika mahusiano kama wenzake anavyowasikia wakisema. Au umempa manung’uniko na ganzi ya moyo?
Ikiwa hukulazimishwa kuingia katika mahusiano na uliyenaye hupaswi kumfanyia hivyo. Mapenzi ni faraja na burudani, sasa kwanini unamfanyia hivyo mwenzako?
Hivi ulishawahi kujiuliza hatima ya lawama za kila siku za mpenzi wako dhidi ya matendo yako yasiyoonesha dalili za mapenzi wala kumjali? Tengeneza picha ya kitakachotokea baada ya mpenzi wako kuchoshwa na hali hiyo. Hakuna binadamu anayependa kuteseka ikiwa kuna sehemu anahisi atapata faraja na amani ya nafsi.
Je, vipi kauli zako kwa mpenzi wako ni zile za kujenga tabasamu katika sura yake au ni maudhi na fujo kwa kwenda mbele? Unamfanya mwenzako afurahi karibu kila neno linalotoka katika kinywa chako, au ndiyo ukianza kuongea tu unamfanya alie na kujutia hatua yako ya kufungua mdomo?
Maneno yako yanachangia asilimia ngapi ya furaha katika maisha yake? Au ndiyo asilimia kubwa ya huzuni zake zipo katika maneno yako.
Unampa sababu ya kukuamini? Au ndiyo ukitoka tu yeye tumbo joto akifikiria kile alichokikuta katika simu yako! Yuko hivyo? Chunga sana.
Ulishawahi kujiuliza mwisho wa wasi wasi wake kwako nini? Unadhani kuna mtu anapenda kila siku kuwa roho juu? Fikiri upya kuhusu hili.
Wengi waliosalitiwa na wapenzi pia sababu hii imo. Walivyoona wapenzi wao hawawaelewi waliamua kujipa pumziko la moyo kwa wengine, kwa kile walichoaimini kama kupunguza aina ya f’lani ya wasiwasi kwa maana kama ni ubaya basi wote watakuwa wakifanyiana.
Kuwa makini zaidi katika mahusiano yako ikiwa kweli unahitaji amani na burudani halisi. Ni mara ngapi mpenzi wako amewahi kukutilia mashaka na f’lani hapo mtaani au kazini? Unadhani ni kwanini ana mashaka hayo? Bila shaka ni ukaribu wenu uliojaa maswali. Ukaribu unaomnyima raha na amani katika nafsi yake, kiasi cha kufanya ahisi anaibiwa mali yake.
Unaridhiwa na wasiwasi wa mpenzi wako? Kwanini huchukui hatua za kumfanya ajue ukweli halisi badala ya kumuacha aendelee kuteseka kwa mawazo na hangaiko la nafsi kama si kweli?
Muite mpenzi wako pamoja na yule anaye mshuku kisha mueleze ukweli halisi kama kweli mawazo yake si sahihi juu yenu.
Kumuacha mpenzi wako apate msukosuko wa nafsi juu ya fikra zake juu ya ukaribu wenu ni kumfanya kuamini kuwa ni kweli ‘mnatoka’ pamoja. Hata wewe bila shaka ungeamini hivyo ingekuwa ni wewe.
Kuziacha hisia zake kuteseka ni kuonesha kutomjali wala na kumthamini. Katika hali yoyote onesha thamani yake kwako kwa matendo yako mazuri naya kutia faraja. Katika kila bonde weka sawa ili mapenzi yenu yazidi kushamiri na kuongeza furaha baina yenu.
0 Response to "FANYA HAYA KWA FAIDA YA MAPENZI YAKO"
Post a Comment